Changamoto za Mikakati ya Upole katika Mazungumzo ya Vipindi vya Sobetab Kapchi katika Idhaa ya KASS FM

Citation:

Muge, T., 2018. Changamoto za Mikakati ya Upole katika Mazungumzo ya Vipindi vya Sobetab Kapchi katika Idhaa ya KASS FM. Mara Research Journal of Kiswahili - ISSN 2520-0577, 3, p.47–57.

Abstract:

Jamii ina mikakati mbalimbali ambayo hutumika wakati wa mazungumzo. Mikakati hiyo ni ya upole na ina kanuni kadhaa kuhusu namna ya kuwasiliana. Upole ni utambuzi ambao mtu humwonyesha mwingine kwa kuzingatia au kuepuka kaida au desturi fulani za mazungumzo. Ni hali ya kuonyesha heshima kwa washiriki wengine katika mazungumzo. Mikakati ya upole ni mbinu wanazobuni na kuzingatia wahusika wa mazungumzo ili ‘kuokoa nyuso’ zao. Makala haya yalinuia kuchanganua changamoto zinazosawiriwa na wahusika wa mazungumzo ya Sobetab Kapchi (Maisha ya Jamii) wakati wa utekelezaji wa kanuni za upole. Uchunguzi uliongozwa na Nadharia ya Upole, hasa mhimili wa ‘kuokoa uso’, kama ilivyopendekezwa na Brown na Levinson. Sampuli iliteuliwa kimakusudi kwa kunasa vipindi vinne vya Sobetab Kapchi (SK) ili kupata data za uchanganuzi. Mwisho, hoja zinazohusiana na upole zilinakiliwa na kuwekwa kwenye makundi manne ya mikakati ya upole ili kuchanganuliwa. Makundi hayo ni ya mkakati wa kuwa kwenye rekodi, mkakati wa upole chanya, mkakati wa upole hasi na mkakati wa kuwa nje ya rekodi. Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaelezo kwa kutumia mazungumzo ya washiriki kama mifano halisi. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa wahusika wa mazungumzo ya SK hukumbana na changamoto nyingi wanapotekeleza mikakati ya upole wakati wa mazungumzo.

Website